| Habari za Kitaifa (source Habari Leo)Makabwela kunufaika na bima nafuu ya afya Imeandikwa na Namsembaeli Mduma; Tarehe: 6th December 2010 @ 23:40 visits http://www.habarileo.co.tz/kitaifa/?n=12295 |
|||||||||
WATANZANIA wa kipato cha chini wataanza kunufaika na bima mpya ya afya ya bei nafuu kutoka kwa Wakala wa Kwanza wa Bima Ndogo itakayoanza kutolewa kwa majaribio Dar es Salaam hivi karibuni, ili kuwaondoa katika hatari ya kupoteza maisha kwa maradhi, kutokana na kipato duni chao. Akizungumza wakati wa uzinduzi wa bima hiyo Dar es Salaam jana, Meneja Mradi wa wakala huo, Wilson Mnzava alisema sambamba na bima hiyo ya afya, Watanzania hao watanufaika na bima nyingine ya Kilimo Kwanza na ile ya mikopo itakayowafanya warejee katika hali zao za kawaida, baada ya kupata matatizo yatakayosababisha washindwe kurejesha mikopo watakayokuwa wamekopa kutoka kwa wakopeshaji wao. Mnzava alisema bima hiyo ya afya inalenga kuiunga mkono Serikali katika vita yake dhidi ya maradhi na vifo vinavyosababishwa na hali duni ya kipato cha mwananchi inayomfanya ashindwe kumudu gharama za matibabu. Alisema wakala wao anahudumia Watanzania watakaokuwa wamejiunga kwenye vikundi vya watu wasiopungua watatu ambao watakuwa wanajihusisha na vikundi vya uzalishaji kama vile Saccos, benki au vingine vya biashara. Alisema gharama watakayotozwa kwa mwezi ni Sh 3,500 hadi 4,000 tu na kwamba watakuwa na haki ya kuuelekeza wakala endapo wanataka kulipiwa matibabu hospitalini au kulipwa fedha. Katika hilo bima hiyo na nyingine ya afya, alisema kwa siku saba atakazokuwa amelazwa mteja wao na kuamua familia yake ilipwe, bila kujali atakaa hospitali kwa muda gani, atalipwa Sh 10,000 kila siku kwa siku saba, na hiyo itafanywa kwa kila mwana familia yakeatakayeugua. Huduma nyingine ya bima iliyozinduliwa ni ile ya Kilimo Kwanza ambapo mwananchi mwenye mazao yatakayokuwa yameathiriwa na janga lolote, atalipiwa gharama alizokopa kwa ajili ya kilimo hicho. Kadhalika, kwa wale wenye mikopo katika asasi au benki mbalimbali nao watalipiwa mikopo yao pale watakapokuwa wamepata vilema vya maisha au kupoteza maisha, au sababu zingine zitakazowafanya washindwe kuendelea kulipa mikopo hiyo. “Hii ni faida kwa Watanzania, tumeanza kufanya hivyo kwa benki ya wanawake miaka miwili iliyopita, tumewekea bima mikopo ya wanavikundi wao waliojiunga nasi,” alieleza Mnzava. wwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwwww |
